Wednesday, October 21, 2015

MAMBO YA KUZINGATIA SIKU YA UCHAGUZI 25-10-2015

Tume ya uchaguzi imeaanisha mambo muhimu ya kuzingatia,ili kujiepusha na matatizo ni vyema usome na kuzingatia uchaguzi wa mwaka huu una msisimko mkubwa kati ya Watanzania.


      



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAELEKEZO KWA MAMBO YASIYORUHUSIWA KUFANYIKA SIKU YA KUPIGA KURA
1.   UTANGULIZI
Malekezo haya yametolewa chini ya kifungu cha 126 na kifungu cha 63 (2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 63 (2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura 292.
Kwa kuzingatia Sheria na Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 kama yalivyochapishwa kwenye TANGAZO LA SERIKALI NA 294 la tarehe 27 JULAI 2015 Vyama vya Siasa na Wagombea wanatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:-
1)     Kuheshimu na kutekeleza Sheria za Uchaguzi, Kanuni za Uchaguzi, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na Sheria zingine za Nchi katika kipindi chote cha Uchaguzi.
2)     Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wagombea wawaelimishe Wanachama wao kutekeleza Sheria za Uchaguzi, Sheria zingine za Nchi, Kanuni na taratibu zilizopo.
3)     Vyama vyote vya Siasa, Wagombea Wanachama na Wafuasi wa Vyama vya Siasa wahakikishe kwamba Wanafanya hatua za makusudi:
3.1.      Kufanya Uchaguzi ulio huru na haki.
3.2.      Kukataa na kulaani vitendo vya vurugu na vitisho
3.3.      Kueneza taarifa sahihi kuhusiana na mchakato wa Uchaguzi
4)     Vyama vyote vya Siasa na Wagombea wajenge mazingira ambayo yatawezesha Uchaguzi kufanyika kwa uhuru na haki na kuhakikisha wanashirikiana na Watendaji wa Uchaguzi kuhakikisha upigaji kura  unakuwa wa amani na utulivu ili Wapiga kura wawe huru kutumia haki yao ya kupiga kura bila usumbufu, bughudha au vitisho.
Ili wapiga kura waweze kupiga kura bila usumbufu, bughudha, vitisho au woga wa aina yoyote, Kifungu cha 63(2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura Na. 343 na Kifungu cha 63 (2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura Na. 292 imeelezwa bayana watu wanaoruhusiwa kuwepo katika vituo vya kupigia, kuhesabu na kujumlishia kura. Watu hao ni:-
              1.   Msimamizi wa Kituo.
              2.   Msimamizi Msaidizi wa kituo.
              3.   Mgombea.
              4.   Wakala wa upigaji kura.
              5.   Mpiga kura kwa ajili ya kupiga tu.
              6.   Mtu anayemsaidia mpiga kura asiyeweza kupiga kura mwenyewe.
              7.   Mtazamaji wa uchaguzi aliyeidhiniswa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa maandishi.
              8.   Mjumbe wa Tume ya Taifa ya uchaguzi.
              9.   Mkurugenzi wa Uchaguzi
          10.   Afisa wa Tume
          11.   Msimamizi wa Uchaguzi na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi
          12.   Askari polisi au mlinzi wa Kituo.
          13.   Mratibu wa Uchaguzi wa Mkoa.
Kwa maana hiyo watu wote ambao hawakutajwa kwenye Sheria hiyo hawaruhusiwi kuwepo kwenye maeneo ya kupigia, kujumlishia na kuhesabu kura kwani wenye jukumu la kulinda maslahi ya mgombea na chama chake ni mawakala na Wagombea pamoja na wote waliotajwa kwenye sheria.
2.   MAZOEA YA KUWEPO UMBALI WA MITA 200 AU 300 KUTOKA KITUO CHA KUPIGIA KURA
Kumekuwepo na mazoea kwamba, baada ya kupiga kura wafuasi wa vyama hubakia na kukaa kwenye maeneo ya kupigia kura umbali wa mita 100 au 200 au 300.
Jambo hili ni kinyume na Sheria za Uchaguzi. Kwani, katika kifungu cha 104 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura Na. 343 kinasema nanukuu
“Hakuna mtu atakayefanya Mkutano siku ya kupiga kura au; ndani ya jengo lolote ambamo upigaji kura katika uchaguzi unaendelea, au mahali popote ndani ya eneo la mita miambili ya jingo hilo, kuvaa au kuonyesha kadi ya picha yoyote, upendeleo au nembo nyingine inayoonesha kuunga mkono mgombea Fulani katika uchaguzi”
Mwisho wa kunukuu.
Aidha, kifungu cha 103 (1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 kinasema, Nanukuu:
“hakuna mtu atakayeruhusiwa, katika jengo lolote ambalo upigaji kura katika uchaguzi unaendelea, au njia yoyote inayotumiwa na umma ndani ya umbali wa mita mia tatu ya mlango wowote wa kuingilia katika jingo, atavaa au kuonyesha kadi, upendeleo au nembo yoyote inayoashiria kumuunga mkono mgombea Fulani katika uchaguzi”
Mwisho wa kunukuu.
Kifungu cha 5 cha Sheria ya Adhabu, Sura Na. 16 kinaeleza maana ya njia ya Umma. Nanukuu:
“Public way includes any highway, market place, square, street, bridge or other way which is lawfully used by the public”
Mwisho wa kunukuu.
Vifungu vya Sheria zote kwa pamoja havisemi wala kutoa fursa au nafasi kwa wananchio kukusanyika zinapiga marufuku na kukataza uvaaji wa sare, au nembo au alama za Vyama vya Siasa siku ya kupiga kura kwa umbali kati ya mita 200 na 300.
Hivyo basi ieleweke kwamba umbali huo wa mita 200 mpaka 300 sio umbali unaowaruhusu watu kukusanyika kwa kisingizio cha kulinda kura.
Aidha, uzoefu unaonesha kwamba, katika kampeni zinazoendelea, pale ambapo wafuasi wa vyama tofauti wanapokutana uwezekano wa kutokea vurugu ni mkubwa na sehemu nyingine vurugu zimetokea na kusababisha maafa majeruhi na uharibifu mali.
Hivyo, endapo kila Chama kitaamua kuwaelekeza wafuasi wake kubaki kwenye vituo vya kupigia kura uwezekano wa kutokea vurugu ambazo zinaweza kupelekea kuwatishia, kuwabugudhi, kuwatia hofu na kuwasumbua wapiga kura ni mkubwa hivyo kuhujumu zoezi la upigaji kura.
Katika juhudi na dhamira ya kuwa na uchaguzi huru na haki kwenye mazingira ya usalama na Amani, Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha 126 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura Na. 343 inatoa maelekezo yatakayoweka mazingira mazuri ya kufanya uchaguzi.
Hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatoa maelekezo yafuatayo katika Siku ya kupiga Kura:
1)     Ni marufuku kwa mtu yeyote kukaa bila ya sababu ya msingi katika vituo vya kupigia, kuhesabu na kujumlishia kura kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria ya uchaguzi.
2)     Kila Mpiga kura akishapiga kura haruhusiwi kuwepo kwenye eneo lolote la vituo vya kupigia kura ndani.
3)     Kuendelea kubaki kwenye kituo cha kupigia kura bila kuwa miongoni mwa watu wanaotambuliwa na Sheria ni kukiuka Sheria ya Uchaguzi.

KURA YAKO NI MUSTAKBARI WAKO, JITOKEZE KUPIGA KURA TAREHE 25 OKTOBA, 2015

Imetolewa na:

Kailima R. Kombwey
MKURUGENZI WA UCHAGUZI

09 OKTOBA, 2015

0 comments:

Post a Comment