Thursday, December 3, 2015

MAJALIWA AFUMUA UOZO MWINGINE BANDARINI NA SHIRIKA LA RELI,PATA TAARIFA YOTE HAPA





WAZIRI
MKUU ATINGA TENA BANDARINI NA TRL


*Akuta makontena 2,431
yametoka bila kulipiwa ushuru


*Ataka majina yaletwe
ofisini leo saa 11 jioni


*Atoa wiki wiki moja
kwa mfumo wa malipo kubadilishwa


*Akagua mabehewa, awaweka
kiporo TRL





WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara
nyingine ya kushtukiza bandarini na kukagua mfumo wa upokeaji na utoaji mizigo
na utozaji wa malipo baada ya kupewa taarifa kwamba kuna makontena 2,431
yametolewa bila kulipiwa ushuru.Waziri Mkuu alisema kwa mujibu wa taarifa ya
ukaguzi wa bandari ya kuanzia Machi hadi Septemba 2014, makontena hayo yalipita
bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu nne (ICDs) ambazo ni JEFAG, DICD, PMM
na AZAM.Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni watumishi 10
tu ambao wamesimamishwa kazi kutokana na makosa hayo. “Mmeamua kuwasimamisha
kazi watu wadogo na kuwaacha wakubwa wanaendelea na kazi. Hatuwezi kuendelea kuikosesha
Serikali mapato namna hii,” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amemtaka Kaimu Meneja wa
Bandari, Bw. Hebel Mhanga amletee ofisini majina ya watumishi wote waliohusika
na ukwepaji kodi huo ifikapo leo saa 11 jioni. Pia amempa Meneja huyo wiki moja
kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo kutoka kwenye
billing system na badala yake kuweka mfumo
wa malipo wa kielektroniki (e-payment).

Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Desemba 3,
2015), wakati akikagua idara mbalimbali za mamlaka ya bandari na kuona ukaguzi
wa mizigo unavyofanyika kwa kutumia scanners. Akiwa kwenye chumba cha scanner mojawapo, Waziri Mkuu alikuta manifest moja ikisema kontena limejaa diapers lakini picha ya kwenye kompyuta ya
scanner ilionyesha kuwa ndani ya kontena
hilo kuna vitu kama vifaa vya umeme.


Kwa mujibu wa Kaimu Meneja Bandari upande wa
Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Bw. Ben Usaje ambaye pia ni msimamizi wa kitengo cha scanner, inapobainika taarifa kama hiyo
inapaswa itumwe kwa wenye ICDs ili wafanye ukaguzi kwa kulifungua kontena ili
kuhakikisha mali zilizomo ndizo zilizoandikishwa kwenye manifest.

Katika
hatua nyingine,
Waziri Mkuu Majaliwa amefanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za Shirika la
Reli (TRL) na kukagua mabehewa yaliyokuwepo kisha akazungumza na baadhi ya wafanyakazi
waliokuwepo kwenye stesheni hiyo ambako alibaini madudu kwenye malipo ya
mishahara na makato ya michango ya wafanyakazi.

Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu TRL, Mhandisi
Elias Mshana, Waziri Mkuu alisema amefika kwenye shirika hilo ili kujifunza
utendaji wao kazi lakini anazo taarifa za wao kupewa fedha na Serikali kiasi
cha sh. bilioni 13.5/- ili waendeleze miundombinu ya reli lakini hawakufanya
hivyo. “Nia ya kuwapa fedha hizo ilikuwa ni kuboresha miradi ili muweze
kujiendesha kibiashara lakini nyie mkaamua kujilipa wenyewe,” alisema.

“Ninazo taarifa kuwa baada ya hapo, mlikopa
sh. bilioni 3 kutoka benki ya TIB ili kuendesha miradi ya shirika lakini badala
ya kufanya miradi, fedha hizo mkaamua nazo kujilipa mishahara. Sasa sijui
mnarudishaje huo mkopo wakati hakuna mradi wowote uliofanyika,” alihoji bila
kupata majibu.

Alipoulizwa wafanyakazi wana matatizo gani
hapo TRL, Katibu wa TRAWU, Bw. Boaz Nyakeke alisema wanadai malimbikizo ya
makato yao kwenye mifuko ya pensheni, malimbikizo ya makato kwenye SACCOS na malimbikizo
ya kuanzia Julai – Novemba 2014.


Waziri Mkuu kwa upande wake alimtaka
Mhandisi Mshana asimamie uboreshaji huduma za usafiri wa treni katika Jiji la
Dar es Salaam ili hata mabasi ya mwendo kasi yatakapoanza wananchi waweze kuwa
na uhuru wa kuchagua aina ya usafiri wautakao.

“Tunataka kujenga yadi kubwa nje ya mji ili watu
wenye magari wawe wanayaacha huko na kutumia usafiri wa treni au DART kuja
mjini kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es
Salaam,” alisema.

0 comments:

Post a Comment