Monday, November 2, 2015

MAMLAKA YA HALI YA HEWA YATOA ANGALIZO JUU YA MWENENDO WA MVUA ZA VULI-2015


Tokeo la picha la tma tanzania meteorological agency LOGO



MIFUMO YA HALI YA HEWA

Kuendelea kuongezeka kwa joto katika maeneo ya Bahari ya Pasifiki kunaonesha kuimarika kwa El-Nino katika Bahari ya Pasifiki kama ilivyoelezwa katika taarifa ya Mamlaka iliyotolewa mapema mwezi Septemba, 2015. Hata hivyo, mifumo mingine ya hali ya hewa ikiwemo mwitikio wa mfumo ya hali ya hewa katika Bahari ya Hindi imekuwa na mchango hasi kinyume na ilivyotarajiwa katika mwenendo wa mvua za Vuli nchini katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2015 na kusababisha vipindi virefu vya upungufu wa mvua katika Mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
Hata hivyo mifumo ya hali ya hewa katika Bahari ya Hindi katika ukanda wa Afrika Mashariki na ukanda wa pwani ya Angola katika Bahari ya Atlantiki imenza na inaendelea kuimarika. Kuimarika kwa mifumo hii kunatarajiwa kusababisha kunyesha kwa mvua katika maeneo mengi kama zilivyotabiriwa katika kipindi cha mwezi Novemba-Disemba 2015. Kwa upande mwingine, mpaka sasa baadhi ya maeneo ya Mikoa ya Ukanda wa Ziwa Viktoria yameendelea kupata mvua za wastani katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2015.


MVUA KWA MWEZI NOVEMBA HADI DISEMBA 2015

Maeneo ya Ukanda wa Ziwa Viktoria, Kanda ya Magharibi na Nyanda za juu kaskazini Mashariki yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani katika kipindi cha mwezi Novemba hadi Disemba 2015, pamoja na vipindi vifupi vya mvua kubwa. Kwa ujumla mwelekeo wa mvua bado ni kama ulivyotolewa mapema tarehe 2 Septemba 2015.
Maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka Mikoa ya Dodoma, Singinda, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Songea, Mbeya, Iringa, Njombe, Tabora, Kigoma Rukwa na Katavi mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya pili na ya nne ya mwezi Novemba, 2015. Ambapo mvua hizo zimeanza kujiimarisha katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi na zinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengine mwezi huu wa Novemba 2015. Hata hivyo, Wilaya za Kondoa, Kongwa na Singida Vijijini katika mikoa ya Dodoma na Singida zinatarajiwa pia kupata vipindi vya mvua mapema mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2015.

0 comments:

Post a Comment